MAANDAMANO ya amani yaliyokuwa yameandaliwa na chama cha
demokrasia na maendeleo(chadema) yamegeuka shubiri kwa wakazi wa jiji la Mwanza
baada ya kuibuka mapambano makali baina ya waandamanaji hao na jeshi la polisi
mkoani Mwanza na kusababisha polisi kutumia nguvu kuwatawanya wafuasi wa chama
hicho.
Maandamano hayo ya amani ambayo yalianzia katika eneo la Buzuruga
nje kidogo ya jiji la Mwanza yalikuwa yakiongozwa na wabunge Highness
Kiwia wa Ilemela pamoja na Ezekiel Wenje kuelekea katika viwanja vya
Furahisha na yalilenga kumshinikiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Ernest
Ndikilo kutoa barua zinazodaiwa kuandikwa na ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi
kuwarejesha madiwani watatu waliotimuliwa katika Manispaa ya Ilemela kutokana
na kushindwa kuhudhuria vikao vitatu mfululizo.
Polisi wenye silaha pamoja na askari kanzu walianza kutanda katika
eneo hilo la Furahisha wakiongozwa na Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa
wa Mwanza RCO Konyo ambaye alikuwa akitumia gari lenye namba za usajili DK
068EXV aina ya Toyota Land Cruiser
Maandamano hayo ambayo awali yalionekana kana kwamba
yangelimalizika salama yaliwasili katika viwanja vya Furahisha majira ya saa
5.38 huku yakiongozwa na gari la polisi lenye namba za usajili za nchi ya
Uganda 779 UAG likiwa nimesheheni polisi wenye silaha nzito ikiwa ni
pamoja na mabomu ya machozi na bunduki pamoja na askari kadhaa ambao walikuwa
katikati ya maandamano hayo.
Baada ya maandamano hayo kuwasili katika viwanja vya Furahisha kwa
amani,waandamani hao ambao walikuwa na mabango mbalimbali yaliyosomeka
kuwa :‘Matata hatutaki uendelee kuwa Meya wa Ilemela rudia kazi yako ya
awali,.... na jingine Jaji Sumari tumechoka kuahirisha mara
kwa mara kesi dhidi ya Matata ....na
jingine lililosomeka kuwa RD Ndikilo tunahitaji barua za
kurejeshwa kwa madiwani wetu.
Hata hivyo tofauti na ilivyokuwa imetangazwa kuwa maandamano hayo
ya amani yangelipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ernest Ndikilo,hakukuwa na
kiongozi yoyote wa Serikali ambaye alikuwepo uwanjani hapo kupokea maandamano
hayo.
Kufuatia kutoonekana kwa kiongozi yoyote wa Serikali,viongozi wa
chadema pamoja na wabunge wao walikutana kwa faragha kwa dakika kadhaa kwa
ajili ya kujua hatima ya maandamano hayo ambapo Mbunge wa Nyamagana Ezekiel
Wenje alipanda jukwaani saa 6.45 na kuwaeleza maelfu ya waandamanaji kuwa
wameamua kumtuma Mbunge wa Ilemela Highnes Kiwia kwenda ofisini kwa Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza kuchukua majibu kwa ajili ya kuwaletea wananchi walioandamana juu
ya hatima ya madiwani hao.
Hata hivyo saa moja baadae Mbunge huyo alisimama jukwani na
wakuwaeleza waandamani hao kuwa simu ya Mbunge Kiwia ilikuwa haipatikani hivyo
kuwataka kuandamana kwenda kwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza kujua kulikoni na hapo
ndipo hali ya hewa ilipochafuka.
Jeshi la polisi baada ya kuona wandamanaji hao wameanza kuelekea
katika ofisi za Mkuu wa mkoa liliwataka kutawanyika ambapo waandamanaji hao
walikaidi ndipo jeshi la polisi lilipoamua kutumia mabomu ya machozi
kuwatawanya wafuasi hao.
Vurugu hizo ambazo zilianza majira ya saa 7.30 zilisababisha
kufungwa kwa baadhi ya barabara kutokana na waandamanji hao kuweka vizuizi vya
mawe na kuchoma matairi,ambapo pia maduka na ofisi mbalimbali zililazimika
kufungwa kwa muda kupisha vurugu hizo.
Baadhi ya wananchi ambao walikuwa wakitumia usafiri wa umma
walionekana wakishuka kupitia katika madirisha ya magari hayo na kukimbia kwa
hofu ya kujeruhiwa na mabomu pamoja na mawe ambayo yalikuwa yakirushwa na
waandamanji hao kwa jeshi la polisi.
MKUU WA MKOA WA MWANZA ALONGA.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza akizungumza na Mbunge Kiwia pamoja na
viongozi wa chadema ofisini kwake alisema kuwa ameshangazwa na uvumi huo kuwa
ofisi yake imekalia barua za kurejeshwa kwa madiwani Abubakar
Kapera(Nyamanoro),Dan Kahungu(Kirumba) pamoja na Marietha Chenyenge(Ilemela).
RC Ndikilo alisema kuwa Serikali imekuwa ikifanya kazi zake kwa
maandishi na sio kwa kufuata maneno ya mtaani na kueleza kuwa hana barua yoyote
toka ofisi ya Waziri Mkuu inayomualifu kuhusu kuwarejesha madiwani hao baada ya
kukata rufaa.
“We Mbunge kuna siku ulinipigia simu ukiniuliza juu ya kuwepo kwa
barua hizo nami nilikujibu kuwa kwa kuwa uko hapo Bungeni Dodoma ambapo pia
kuna ofisi ya Waziri Mkuu nilikujibu kuwa ni muhimu ukawaona viongozi wakuu wa
Tamisemi ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu,pia nilikushauri kuwa wakupe japo
nakala ya barua hiyo”,alisema RC Ndikilo.
“Lakini cha kushangaza nimekuwa nikisikia maneno ya ajabu kuwa
nimeficha barua za madiwani hao,ikumbukwe kuwa madiwnai hao hawakukata rufaa
kwangu bali walikata rufaa ngazi ya juu kabisa,ili kukata mzizi wa fitina
naomba kati ya tarehe 26 hadi 27 wewe Mbunge pamoja na mimi twende TAMISEMI
kukutana na viongozi ili kukata mzizi wa fitina na tuje tuwaeleze wananchi
ukweli uliopo”,alisema RC Ndikilo.
Kuhusu suala la Meya Henry Matata kutoondolewa madarakani RC
Ndikilo alisema kuwa hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuheshimu mamlaka ya
mahakama na kuwataka chadema kuvuta subira hadi pale mahakama itakapotoa
maamuzi yake.
KAULI YA MBUNGE KIWIA.
Akizungumza katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Kiwia alisema
kuwa waliamua kuitisha maandamano hayo kutokana na kuelezwa na Waziri Hawa
Ghasia kuwa tayari barua hizo zimeishatumwa mkoani Mwanza.
“Mheshimiwa Mkuu wa mkoa hawa madiwani waliosimamishwa ni
wawakilishi wa wananchi,wamekaa nje kwa miezi saba sasa na uchaguzi wa Meya
haukuwa halali ndio maana tuliamua kuitisha maandamano kwa ajili ya kuhakikisha
madiwani hawa wanarejeshwa.
RPC MANGU.
Akizungumza kwa simu juu ya kutokea kwa vurugu zilizosababisha
kupigwa kwa mabomu ya machozi,Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Ernest
Mangu alisema kuwa polisi walifanikiwa kudhibiti vurugu hizo na hadi sasa
hawezi kusema ni wananchi wangapi ambao walikamatwa kuhusu vurugu hizo.
No comments:
Post a Comment