MAWAZIRI watatu wako
mkoani Iringa na leo Mei 24 wanatarajia kushiriki kikao nyeti kinachohusu
mustakabali wa ujenzi wa stendi mpya ya mabasi yaendayo mikoani katika eneo la
Igumbilo.
Mawaziri hao ni
pamoja na Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Mazingira Dk
Benelith Mahenge na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
Hawa Ghasia.
Maamuzi
yatakayotolewa katika kikao hicho kitakachofanyika katika ukumbi wa manispaa ya
Iringa yatatoa majibu ambayo kwa namna moja au nyingine yataupa ushindi upande
fulani wa siasa.
Wakati halmashauri ya
manispaa ya Iringa na madiwani wake wote wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanataka
stendi hiyo ijengwe katika eneo hilo, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini,
Mchungaji Peter Msigwa na madiwani wenzake wawili wanaoingia katika baraza hilo
wakitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanapinga ujenzi huo.
Hata kama sababu za
kisiasa zitapingwa kutumika katika maamuzi yatakayotolewa katika kikao hicho,
upande utakaoshinda unaweza kujiongezea au kujipunguzia mtaji katika mchakato
wa vyama hivyo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Hivi karibuni, Waziri
wa Mazingira, Dk Mahenge alifanya ziara mjini Iringa na kuizuia manispaa hiyo
kuendelea na shughuli zozote za kuendeleza eneo hilo kwa madai kwamba kwa
nyakati toafuti mara tatu, amepokea malalamiko kutoka kwa mdau mkuu wa maji,
wizara ya maji, ikitaka ujenzi wa stendi hiyo usitishwe kwa hofu kwamba
unaweza kuharibu mazingira ya eneo hilo pamoja na mto Ruaha mdogo unaopita
hapo.
Dk Mahenge akaliagiza
Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya upya tathmini ya
athari ya mazingira katika eneo hilo.
Agizo hilo
lilitafsiriwa na wadau wanaofuatilia sakata hilo ikiwemo Blog hii kwamba
tathmini ya athari za mazingira iliyofanywa na manispaa hiyo kupitia
Mtaalamu Mshauri wa
Mazingira aitwaye Arms on Environemnt Ltd ya Dar es Salaam ilikuwa na walakini.
Kwa kupitia thathmini
ya mtaalamu huyo halmashauri hiyo iliruhusiwa kujenga stendi hiyo kwa maelezo
kwamba hakutakuwa na athari yoyote katika mto Ruaha Mdogo kwasababu utakuwa
mbali na eneo patakapojengwa stendi hiyo.
Macho na masikio hii
leo yataelekezwa katika kikao hicho na kwa vyovyote iwavyo maamuzi yake
yatakuwa ushindi ama kwa CCM au Chadema.
No comments:
Post a Comment