MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema hafikirii kugombea
urais kwa tiketi ya chama hicho wala ubunge katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Alisema
mwaka 2015, ndio mwaka wa mwisho kujihusisha na siasa ambapo dhamira yake ni
kutafuta chuo ambacho ataweza kufundisha masomo ya uchumi na maliasili.
Bw.
Kabwe aliyasema hayo hivi karibuni katika mahojiano maalumu na gazeti hili siku
chache baada ya viongozi 105 kutoka Vyuo Vikuu 30 nchini, kupendekeza majina ya
wanasiasa wanaofaa kuwania urais mwaka 2015.
Jina
la Bw. Kabwe, lilishika nafasi ya pili katika mchujo huo ambapo Mbunge wa
Bumbuli, mkoani Tanga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Bw. January Makamba, alishika nafasi ya kwanza kwa tiketi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) Mwanasiasa aliyeshika nafasi ya tatu katika mchujo huo
alikuwa Mbunge wa Ubungo, Dar es Salaam, Bw. John Mnyika (CHADEMA).
"Hiki
ni kipindi cha mwisho kwangu kujihusisha na siasa kwani nimechoka nazo,
nitatafuta chuo nikafundishe na kama nitakosa ni bora nikalime michikichi...
sihitaji urais," alisema.
Katika
mkutano wa wanafunzi hao, walisema Bw. Makamba ana sifa zote za kuwa rais wa
nchi kamaatagombea nafasi hiyo mwaka 2015 ili aweze kulikomboa Taifa ambalo
hivi sasa linakabiliwa na matukio mengi ya uvunjifu wa amani.
Wanafunzi
hao walikwenda mbali zaidi na kuyataja baadhi ya matukio hayo kuwa ni pamoja na
vurugu, kutekwa kwa watu wasio na hatia, kufanyiwa vitendo vya ukatili,
kumwagiwa tindikali na kupungua kwa mtangamano wa kijamii.
Mwenyekiti
wa mkutano huo ambao ulifanyika mkoani Morogoro ambaye pia ni Rais wa Serikali
ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Kampasi ya Mbeya, Bw. Theonest Theophil,
alisema Bw. Makamba alipata kura 72 ambapo Bw. Kabwe alipata kura 20.
Bw.
Theophil alisema sifa za kiongozi wanayemtaka kwanza awe kijana mwenye fikra
mpya, atakayeleta matumaini mapya, kuwaunganisha Watanzania, asiyeendekeza
siasa za kikanda, mdini na mkabila.
Sifa
nyingine ni kiongozi mwadilifu asiye na rekodi ya kutuhumiwa mahali popote kwa
vitendo viovu, mtulivu, mwenye busara na anayepima kauli zake.
Source:
Majira
No comments:
Post a Comment