Sunday, August 18, 2013

MADIWANI WALIOTIMULIWA NA CCM WASEMA WAKO TAYARI KUHAMIA CHADEMA.


MADIWANI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliofukuzwa katika Manispaa ya Bukoba, wamesema wako tayari kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kama chama chao kitaendelea na msimamo wa kuwafukuza. 


Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, mmoja wa madiwani hao ambaye alikataa kutaja jina na kata yake, alisema wako tayari kuhamia Chadema muda wowote kama hawatarudishiwa uanachama wao.


Alisema, madiwani wote waliofukuzwa wana msimamo mmoja ambapo wanasubiri vikao vya Kamati Kuu ya CCM ili wajue hatima yao.

Kwa mujibu wa diwani huyo, wanachokifanya wao ni kutetea maslahi ya taifa na wananchi waliowapigia kura, wala siyo kulinda biashara za watu hata kama wanaungwa mkono na uongozi wa CCM.

Msimamo wa madiwani hao, umekuja siku mbili baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, kuwakaribisha Chadema madiwani wote waliofukuzwa katika manispaa hiyo na kwamba kama wakijiunga na chama hicho, watafundishwa siasa za mageuzi.

Mbowe aliwakaribisha madiwani hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Uhuru Mjini Bukoba juzi, katika mwendelezo wa mikutano ya chama hicho ya mabaraza ya wazi yanayojadili rasimu ya Katiba mpya.

Katika mazungumzo yake, Mbowe alikwenda mbali na kusema chama chake kiko tayari kushirikiana na kiongozi wa CCM anayepinga ufisadi kama anavyofanya Mbunge wa Bukoba Mjini, Khamis Kagasheki.

Alipoulizwa kama wamepata mawazo ya kujiunga na Chadema, baada ya kauli ya Mbowe, diwani huyo alisema wao walishakuwa na mawazo hayo, lakini kauli ya mwenyekiti huyo imewaweka huru zaidi.

“Si kama tumeamua sasa, mawazo ya kuhamia Chadema tulikuwa nayo baada ya uongozi wa mkoa kutangaza kutuvua uanachama, lakini kwa kauli ya Mbowe, kutukaribisha rasmi Chadema, ametujengea moyo zaidi.

“Tatizo letu na meya linafahamika kwamba, ni ufisadi wake tulioulalamikia tangu mwaka jana kwenye vikao vya baraza la madiwani, hatukusikilizwa badala yake tunaonekana wasaliti wa chama.

“CCM wanapaswa kujua kwamba, hoja za wapinzani zikiwa sahihi wananchi wanawaunga mkono, vivyo hivyo na sisi hatuwezi kubeza hoja zao kwa sababu tu ni wapinzani, tutaonekana watu wa ajabu.

“Kimsingi, tumefarijika na kauli ya Mbowe, baadhi yetu tulikuwapo katika mkutano wake jana (juzi) pale Uwanja wa Uhuru, ni suala la muda tu mtasikia Bukoba imezaliwa upya,” alisema diwani huyo.

Balozi Kagasheki ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), anatajwa kuwa na uhasama wa kisiasa na kada mwenzake, Anatory Amani ambaye awali wawili hao walikuwa na ushirika wa karibu.

Alipotakiwa kuzungumzia suala la kufukuzwa kwa madiwani hao, Kagasheki alisema yeye hakuwepo katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa kilichowavua uanachama.

Kuhusu taarifa za kutoelewana na Amani, alisema kila mmoja amekuwa na mtazamo wake juu ya mvutano huo.

“Kila mtu ana maoni yake, siwezi kuzuia hisia na maoni ya watu wengine, kila mtu anaweza kutoa maoni atakavyo, ngoja watu waseme,” alisema Kagasheki.

Madiwani wanane waliofukuzwa wanatuhumiwa kushirikiana na wenzao wa upinzani kusaini hati maalumu na kuiwasilisha kwa mkurugenzi wa manispaa, wakimtaka aitishe kikao ili wapige kura ya kumng’oa madarakani Meya Amani.

Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera kilichokaa Agosti 3 mwaka huu, kiliwafukuza uanachama na uongozi madiwani hao akiwamo Mwenyekiti wake wa Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza na Diwani wa Kata ya Kashai.

Wengine waliofukuzwa ni Diwani wa Kata ya Buhembe, Alexander Ngalinda, Samwel Ruhangisa (Kitendaguro), Dauda Kalumuna (Ijuganyondo), Deus Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Richard Gasper (Miembeni) na Murungi Kichwabuta ambaye ni Diwani wa Viti Maalumu.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...