Tuesday, August 20, 2013

DR.SHEIN APANGUA BARAZA LA MAWAZIRI ZANZIBARI,,


Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein amefanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na kupangua idara zilizokuwa zikisimamiwa na wizara mbalimbali na kuunda wizara mpya nne visiwani humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi Dk.Abdulhamid Yahya Mzee, katika mabadiliko hayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kubakia na Wizara 16 kama ilivyokuwa zamani. 


Taarifa hiyo imetaja Wizara mpya zilizoanzishwa ni Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais tawala za mikoa na Idara maalum za SMZ, ambapo Waziri wake atakuwa Haji Omar Kheir, Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora itakayoongozwa na Dk.Mwinyihaji Makame.

Wizara nyingine ni Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma itakayoongozwa na Haroun Ali Suleiman na Wizara ya Fedha ambayo itakuwa chini ya Omar Yusuph Mzee.

Katika mabadiliko hayo idara zilizohamishwa kutoka Wizara moja kwenda nyingine ni idara ya uwezeshaji ambayo imehamishiwa katika Wizara ya Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto ambayo itaongozwa na Waziri Zainab Omar Mohamed.

Idara nyingine ni utumishi wa umma na utawala bora na kuhamishiwa katika ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, shughuli za tume ya mipango zimehamishiwa ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi kutoka Wizara ya Fedha na idara ya uratibu wa shughuli za SMZ Dar es salaam zimehamishiwa ofisi ya Makamu wa pili wa Rais.

Aidha, Dk.Shein amefanya uteuzi wa Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu wakuu katika Wizara hizo mpya na mabadiliko hayo ameyafanya kwa mujibu wa kifungu cha 53 cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Dk.Shein amemteua Joseph Abdallah Meza kuwa Katibu Mkuu Wizara ya tawala za mikoa na idara maalum za SMZ na Naibu wake Mwinyiussi A. Hassan na CDR Julius Nalimy Maziku.

Wengine ni Fatma Gharib Bilal ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Kazi na utumishi wa Umma na Naibu wake Yakuot Hassan Yakuot, Khamis Mussa Omar ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Naibu Katibu Mkuu ni Juma Ameir Hafidh.

Aidha, Dk.Shein pia amemteua Asha Ali Abdulla kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa jamii, vijana, wanawake na watoto na Naibu wake ni Ali Khamis Juma na Msham Abdulla Khamis.

Source: Mwinyi Sadallah,NIPASHE



No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...