HAYA ninayoyaandika leo katika safu hii
yanaweza kuwa si mageni. Inawezekana kabisa ni marudio ya
kilichokwishakuandikwa.
Huenda pia ni mambo yanayoudhi baadhi ya watu
ama kwa maudhui yake au kwa kurudiwarudiwa kwake. Mara nyingi kuhoji mazoea si
jambo linalopokewa vyema hasa na wale wasioona tatizo katika hali ilivyo
(status quo).
Leo ninapenda kudadisi kwa ukaribu zaidi hicho
ninachokiona huko tunakoelekea kama jamii ambako huenda si wengi wetu wanaoona
umuhimu wa kufanya hivyo. Kabla sijaingia katika udadisi huo nirejee kwa kifupi
utangulizi wangu ambao utaweka mawazo yangu ya leo katika muktadha wake kamili.
Nilianza tena safu hii kwa kuzungumza na
historia. Ni dhahiri kwamba usipoijua historia yako ilivyowatesa babu na bibi
zako, basi una hatari kubwa ya kuiruhusu ijirudie katika maisha yako ya usoni.
Nilisema watu weusi (huu msisitizo ni muhimu sana) wamepitia madhila ya kutisha
katika historia. Hata harufu ya damu iliyomwagika katika madhila waliyopitia
bado ingalipo.
Tafadhali rejesha mawazo yako katika historia
ya miaka ya 1800 wakati mzururaji kutoka Ulaya, Karl Peters, alipomdanganya
mtawala Mangungo wa hapa Tanganyika katika mkataba ambao ulimnyang’anya ardhi
kubwa na kuikabidhi kwa wageni ambao baadaye walikuja kuwakalia babu na bibi
zetu vichwani! Leo akina Karl Peters wanaitwa wawekezaji.
Safiri katika njia ya kutoka Kigoma, Tabora
hadi pwani ya Bagamoyo utakutana na nyayo za watumwa waliokuwa wakibebeshwa
pembe za ndovu huku wakiwa wamefungwa minyororo na kuswagwa kama ng’ombe na
mtesaji aliyeshikilia gobore! Leo watesaji wale wanaitwa wawindaji.
Nenda leo Bagamoyo utaonyeshwa mti walipokuwa
wakinyongewa babu zetu waliokataa kwa jeuri kunyanyaswa, kudhihakiwa na
kufanywa watumwa. Usije kushangaa siku moja ukiambiwa mti ule umekatwa kwa
sababu eneo lile limeuzwa kwa mwekezaji atakayejenga hoteli bora zaidi ya
kitalii.
Nenda Songea utakuta kuna mti waliponyongewa
mashujaa wetu wakipinga ukoloni. Mashujaa wale leo wamesahaulika. Siku moja
utaambiwa eneo lile wameuziwa wawekezaji wa kuja kulima jatropha na mti ule wa
kihistoria umekatwa.
Usipoijua historia yako, utarudia makosa.
Katika makala ya wiki iliyopita nilisisitiza sana umuhimu wa sisi (watu weusi)
kujitambua na kuthamini asili yetu. Nikasema ipo haja ya kuanza kwa makusudi
kabisa kuhoji vitu vingi vya kigeni tulivyovishwa na kulishwa tangu enzi za
utumwa hadi ukoloni ili turejee katika asili yetu ikiwa ni ishara muhimu ya
kujithamini.
Baada ya utangulizi huo ninashawishika sasa
kuendelea na udadisi wangu juu ya hatma yetu kama binadamu wenye akili na
utashi wa kuamua na kutenda kama nilivyobainisha katika makala yangu ya wiki
iliyopita. Na ninaanza na maswali kadhaa.
Je, endapo wageni kutoka mabara mengine
hawangefanikiwa kufika Afrika na kuwekeza kwa ubabe fikra zao, imani zao,
tamaduni zao, majina yao, lugha zao, njia zao, majengo yao, mashine zao,
biashara zao, n.k., ina maana tusingekuwa binadamu kamili? (waweza pia
kujiuliza leo hii tungekuwa wapi kimaendeleo?)
Swali la pili: Je, endapo wageni wangelikuja
lakini wakashindwa kuwekeza kwa ubabe fikra zao, imani zao, tamaduni zao,
majina yao, lugha zao, njia zao, majengo yao, mashine zao, biashara zao, n.k.,
na badala yake wakajadiliana na babu na bibi zetu kwa kuheshimiana, ina maana
leo hii tungekuwa kama tulivyo – na fikra zao, imani zao, tamaduni zao, majina
yao, lugha zao, njia zao, majengo yao, mashine zao, biashara zao, n.k.?
Swali la tatu: Je, akina Malkia Nzinga wa Angola, Jenerali
Kinjekitile Ngware na wenziwe; akina Mtemi Mkwawa na mashujaa wengine
waliopigana kiume kukataa
kutawaliwa kibabe, kunyanyaswa, kudhalilishwa, kunyonywa, na kufanywa nusu
watu, wangelifanikiwa katika vita yao takatifu leo hii tusingelikuwa
tunajitambua zaidi? Yaani tusingelikuwa na fikra zetu, imani zetu,
tamaduni zetu, majina yetu, lugha zetu, njia zetu, majengo yetu, mashine zetu,
biashara zetu, n.k.?
Swali la nne: Endapo fikra zetu, imani zetu,
tamaduni zetu, majina yetu, lugha zetu, njia zetu, majengo yetu, mashine zetu,
biashara zetu, n.k. hazikufaa (au kufua dafu) mbele ya fikra zao, imani zao,
tamaduni zao, majina yao, lugha zao, njia zao, majengo yao, mashine zao,
biashara zao, n.k. kulikuwa na sababu gani ya kuwepo upinzani mkali kutoka kwa
akina Malkia Nzinga, Jenerali Kinjekitile, Mtemi Mkwawa, n.k.? Kulikuwa na
sababu gani ya akina Dedan Kimathi, Kenyatta, Nyerere, Nkrumah, Mandela, na
wengineo kupigania uhuru wa mtu mweusi ili ajitawale na kujiamulia mambo yake
na hatma yake mwenyewe?
Swali la tano: Endapo sasa tunaanza kushuhudia
matukio yanayofanana na yale yale ya karne zilizopita kama vile: Kutiliana
mikataba ya kiwizi katika madini na hata ardhi; kutimua wananchi kutoka katika
makazi yao ya asili ili wawekezaji wawekeze na kuwaajiri wazawa wale kama
manamba; endapo sasa tunaanza kushuhudia wananchi wanaojaribu kukataa
kuondolewa katika ardhi yao wakiondolewa kwa nguvu na hata kuchomewa nyumba zao
wakafie mbali; endapo sasa tunaanza kushuhudia wawekezaji wa nje katika madini
wakithaminiwa zaidi na kulindwa zaidi huku watu wetu (ambao akina Mtemi Mkwawa
walipigana hadi kufa ili kuwalinda) wakiitwa majambazi na kuuwawa kwa risasi za
moto;
Endapo sasa tunaanza kushuhudia wageni wengi
(wajukuu wa watesi wetu) wakirejea, kutokana na uwekezaji wao, na kuwa mabwana
huku sie tukigeuka watwana; endapo sasa tumeanza kushuhudia akina Gbagbo na
Kadafi (achilia mbali upungufu wao wa kibinadamu) wakiondolewa madarakani kwa
fedheha na wajukuu wa wakoloni kwa sababu walianza kutetea maslahi ya watwana;
endapo sasa, miaka 50 baada ya uhuru wa nchi zetu wajukuu wa wakoloni wetu
wanasimama na macho makavu na kuwatangazia viongozi wetu (wakiwa wamevaa suti
zao na tai) kwamba kuanzia sasa watakosa misaada ikiwa hawatachukua kwa ujumla
utamaduni wa wakoloni kama ulivyo na bila kuacha kitu!
Ni nani basi anayedhani kwamba sisi watu weusi
tuko salama kwa kufakamia usasa na kudhani kwamba haya ndiyo maendeleo? Wiki
ijayo ninataka kuonyesha kwamba hoja yangu isipotoshwe, kwamba nina chuki na
wawekezaji wageni au wageni kwa ujumla. Kwanza, ninawaheshimu zaidi wageni hao
kwa sababu wao wanajitahidi kufikiri kwa kutumia vichwa vyao. Ninajaribu
kujenga hoja kwa kuitazama historia kwa sababu siamini kama nilisoma somo la
historia ili kujibia mitihani tu.
Pili, nitajaribu kuonyesha kwamba nchi zetu
zinachokifakamia kwa sasa si maendeleo halisi bali makombo na makandokando ya
usasa ambayo kwa namna ya pekee yanatudidimiza katika utegemezi na kuturejesha
katika ukoloni mpya!
- See more at:
http://www.raiamwema.co.tz/tukikumbushana-historia-tutazuia-ukoloni-mpya#sthash.pEigxXfo.dpuf
No comments:
Post a Comment