Saturday, May 24, 2014

NI INDIRECT FIGHT KATI YA CCM NA CHADEMA IRINGA LEO.



MAWAZIRI watatu wako mkoani Iringa na leo Mei 24 wanatarajia kushiriki kikao nyeti kinachohusu mustakabali wa ujenzi wa stendi mpya ya mabasi yaendayo mikoani katika eneo la Igumbilo.

Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Mazingira Dk Benelith Mahenge na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia.

Maamuzi yatakayotolewa katika kikao hicho kitakachofanyika katika ukumbi wa manispaa ya Iringa yatatoa majibu ambayo kwa namna moja au nyingine yataupa ushindi upande fulani wa siasa.


Wakati halmashauri ya manispaa ya Iringa na madiwani wake wote wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanataka stendi hiyo ijengwe katika eneo hilo, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na madiwani wenzake wawili wanaoingia katika baraza hilo wakitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanapinga ujenzi huo.

Hata kama sababu za kisiasa zitapingwa kutumika katika maamuzi yatakayotolewa katika kikao hicho, upande utakaoshinda unaweza kujiongezea au kujipunguzia mtaji katika mchakato wa vyama hivyo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Hivi karibuni, Waziri wa Mazingira, Dk Mahenge alifanya ziara mjini Iringa na kuizuia manispaa hiyo kuendelea na shughuli zozote za kuendeleza eneo hilo kwa madai kwamba kwa nyakati toafuti mara tatu, amepokea malalamiko kutoka kwa mdau mkuu wa maji, wizara ya maji,  ikitaka ujenzi wa stendi hiyo usitishwe kwa hofu kwamba unaweza kuharibu mazingira ya eneo hilo pamoja na mto Ruaha mdogo unaopita hapo.

Dk Mahenge akaliagiza Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya upya tathmini ya athari ya mazingira katika eneo hilo.

Agizo hilo lilitafsiriwa na wadau wanaofuatilia sakata hilo ikiwemo Blog hii kwamba tathmini ya athari za mazingira iliyofanywa na manispaa hiyo kupitia
Mtaalamu Mshauri wa Mazingira aitwaye Arms on Environemnt Ltd ya Dar es Salaam ilikuwa na walakini.

Kwa kupitia thathmini ya mtaalamu huyo halmashauri hiyo iliruhusiwa kujenga stendi hiyo kwa maelezo kwamba hakutakuwa na athari yoyote katika mto Ruaha Mdogo kwasababu utakuwa mbali na eneo patakapojengwa stendi hiyo.


Macho na masikio hii leo yataelekezwa katika kikao hicho na kwa vyovyote iwavyo maamuzi yake yatakuwa ushindi ama kwa CCM au Chadema. 

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...