Monday, August 26, 2013

AFRICA TUNARUDISHWA KWENYE UKOLONI...!!??SOMA,TAFAKARI,,,CHUKUA HATUA,,,


HAYA ninayoyaandika leo katika safu hii yanaweza kuwa si mageni. Inawezekana kabisa ni marudio ya kilichokwishakuandikwa.
Huenda pia ni mambo yanayoudhi baadhi ya watu ama kwa maudhui yake au kwa kurudiwarudiwa kwake. Mara nyingi kuhoji mazoea si jambo linalopokewa vyema hasa na wale wasioona tatizo katika hali ilivyo (status quo).
Leo ninapenda kudadisi kwa ukaribu zaidi hicho ninachokiona huko tunakoelekea kama jamii ambako huenda si wengi wetu wanaoona umuhimu wa kufanya hivyo. Kabla sijaingia katika udadisi huo nirejee kwa kifupi utangulizi wangu ambao utaweka mawazo yangu ya leo katika muktadha wake kamili.

Nilianza tena safu hii kwa kuzungumza na historia. Ni dhahiri kwamba usipoijua historia yako ilivyowatesa babu na bibi zako, basi una hatari kubwa ya kuiruhusu ijirudie katika maisha yako ya usoni. Nilisema watu weusi (huu msisitizo ni muhimu sana) wamepitia madhila ya kutisha katika historia. Hata harufu ya damu iliyomwagika katika madhila waliyopitia bado ingalipo.
Tafadhali rejesha mawazo yako katika historia ya miaka ya 1800 wakati mzururaji kutoka Ulaya, Karl Peters, alipomdanganya mtawala Mangungo wa hapa Tanganyika katika mkataba ambao ulimnyang’anya ardhi kubwa na kuikabidhi kwa wageni ambao baadaye walikuja kuwakalia babu na bibi zetu vichwani! Leo akina Karl Peters wanaitwa wawekezaji.
Safiri katika njia ya kutoka Kigoma, Tabora hadi pwani ya Bagamoyo utakutana na nyayo za watumwa waliokuwa wakibebeshwa pembe za ndovu huku wakiwa wamefungwa minyororo na kuswagwa kama ng’ombe na mtesaji aliyeshikilia gobore! Leo watesaji wale wanaitwa wawindaji.
Nenda leo Bagamoyo utaonyeshwa mti walipokuwa wakinyongewa babu zetu waliokataa kwa jeuri kunyanyaswa, kudhihakiwa na kufanywa watumwa. Usije kushangaa siku moja ukiambiwa mti ule umekatwa kwa sababu eneo lile limeuzwa kwa mwekezaji atakayejenga hoteli bora zaidi ya kitalii.
Nenda Songea utakuta kuna mti waliponyongewa mashujaa wetu wakipinga ukoloni. Mashujaa wale leo wamesahaulika. Siku moja utaambiwa eneo lile wameuziwa wawekezaji wa kuja kulima jatropha na mti ule wa kihistoria umekatwa.
Usipoijua historia yako, utarudia makosa. Katika makala ya wiki iliyopita nilisisitiza sana umuhimu wa sisi (watu weusi) kujitambua na kuthamini asili yetu. Nikasema ipo haja ya kuanza kwa makusudi kabisa kuhoji vitu vingi vya kigeni tulivyovishwa na kulishwa tangu enzi za utumwa hadi ukoloni ili turejee katika asili yetu ikiwa ni ishara muhimu ya kujithamini.
Baada ya utangulizi huo ninashawishika sasa kuendelea na udadisi wangu juu ya hatma yetu kama binadamu wenye akili na utashi wa kuamua na kutenda kama nilivyobainisha katika makala yangu ya wiki iliyopita. Na ninaanza na maswali kadhaa.
Je, endapo wageni kutoka mabara mengine hawangefanikiwa kufika Afrika na kuwekeza kwa ubabe fikra zao, imani zao, tamaduni zao, majina yao, lugha zao, njia zao, majengo yao, mashine zao, biashara zao, n.k., ina maana tusingekuwa binadamu kamili? (waweza pia kujiuliza leo hii tungekuwa wapi kimaendeleo?)
Swali la pili: Je, endapo wageni wangelikuja lakini wakashindwa kuwekeza kwa ubabe fikra zao, imani zao, tamaduni zao, majina yao, lugha zao, njia zao, majengo yao, mashine zao, biashara zao, n.k., na badala yake wakajadiliana na babu na bibi zetu kwa kuheshimiana, ina maana leo hii tungekuwa kama tulivyo – na fikra zao, imani zao, tamaduni zao, majina yao, lugha zao, njia zao, majengo yao, mashine zao, biashara zao, n.k.?
Swali la tatu: Je, akina Malkia Nzinga wa Angola, Jenerali Kinjekitile Ngware na wenziwe; akina Mtemi Mkwawa na mashujaa wengine waliopigana kiume kukataa kutawaliwa kibabe, kunyanyaswa, kudhalilishwa, kunyonywa, na kufanywa nusu watu, wangelifanikiwa katika vita yao takatifu leo hii tusingelikuwa tunajitambua zaidi?  Yaani tusingelikuwa na fikra zetu, imani zetu, tamaduni zetu, majina yetu, lugha zetu, njia zetu, majengo yetu, mashine zetu, biashara zetu, n.k.?
Swali la nne: Endapo fikra zetu, imani zetu, tamaduni zetu, majina yetu, lugha zetu, njia zetu, majengo yetu, mashine zetu, biashara zetu, n.k. hazikufaa (au kufua dafu) mbele ya fikra zao, imani zao, tamaduni zao, majina yao, lugha zao, njia zao, majengo yao, mashine zao, biashara zao, n.k. kulikuwa na sababu gani ya kuwepo upinzani mkali kutoka kwa akina Malkia Nzinga, Jenerali Kinjekitile, Mtemi Mkwawa, n.k.? Kulikuwa na sababu gani ya akina Dedan Kimathi, Kenyatta, Nyerere, Nkrumah, Mandela, na wengineo kupigania uhuru wa mtu mweusi ili ajitawale na kujiamulia mambo yake na hatma yake mwenyewe?
Swali la tano: Endapo sasa tunaanza kushuhudia matukio yanayofanana na yale yale ya karne zilizopita kama vile: Kutiliana mikataba ya kiwizi katika madini na hata ardhi; kutimua wananchi kutoka katika makazi yao ya asili ili wawekezaji wawekeze na kuwaajiri wazawa wale kama manamba; endapo sasa tunaanza kushuhudia wananchi wanaojaribu kukataa kuondolewa katika ardhi yao wakiondolewa kwa nguvu na hata kuchomewa nyumba zao wakafie mbali; endapo sasa tunaanza kushuhudia wawekezaji wa nje katika madini wakithaminiwa zaidi na kulindwa zaidi huku watu wetu (ambao akina Mtemi Mkwawa walipigana hadi kufa ili kuwalinda) wakiitwa majambazi na kuuwawa kwa risasi za moto;
Endapo sasa tunaanza kushuhudia wageni wengi (wajukuu wa watesi wetu) wakirejea, kutokana na uwekezaji wao, na kuwa mabwana huku sie tukigeuka watwana; endapo sasa tumeanza kushuhudia akina Gbagbo na Kadafi (achilia mbali upungufu wao wa kibinadamu) wakiondolewa madarakani kwa fedheha na wajukuu wa wakoloni kwa sababu walianza kutetea maslahi ya watwana; endapo sasa, miaka 50 baada ya uhuru wa nchi zetu wajukuu wa wakoloni wetu wanasimama na macho makavu na kuwatangazia viongozi wetu (wakiwa wamevaa suti zao na tai) kwamba kuanzia sasa watakosa misaada ikiwa hawatachukua kwa ujumla utamaduni wa wakoloni kama ulivyo na bila kuacha kitu!
Ni nani basi anayedhani kwamba sisi watu weusi tuko salama kwa kufakamia usasa na kudhani kwamba haya ndiyo maendeleo? Wiki ijayo ninataka kuonyesha kwamba hoja yangu isipotoshwe, kwamba nina chuki na wawekezaji wageni au wageni kwa ujumla. Kwanza, ninawaheshimu zaidi wageni hao kwa sababu wao wanajitahidi kufikiri kwa kutumia vichwa vyao. Ninajaribu kujenga hoja kwa kuitazama historia kwa sababu siamini kama nilisoma somo la historia ili kujibia mitihani tu.
Pili, nitajaribu kuonyesha kwamba nchi zetu zinachokifakamia kwa sasa si maendeleo halisi bali makombo na makandokando ya usasa ambayo kwa namna ya pekee yanatudidimiza katika utegemezi na kuturejesha katika ukoloni mpya!

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/tukikumbushana-historia-tutazuia-ukoloni-mpya#sthash.pEigxXfo.dpuf


No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...