Tuesday, February 25, 2014

KALENGA; GODFREY MGIMWA AICHUKIA CHADEMA KWA SERA ZA KIBAGUZI NA KUMCHAFUA.


MGOMBEA Ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mdogo Jimbo la Kalenga, Iringa Vijijini, Bw. Godfrey Mgimwa, amesema yeye ni Mtanzania halisi na hana chembe yoyote ya Uzungu kama wanavyodai CHADEMA. 

Alisema kama kila Mtanzania anayekwenda kusoma nje ya nchi anapoteza uraia wake, Tanzania itakuwa na wanasiasa wengi wanaokosa sifa ya kuendelea kuwa raia.

Bw.Mgimwa aliyasema hayo juzi katika mkutano wa kwanza wa kampeni za kuwania ubunge wa jimbo hilo ambalo lilikuwa likiongozwa na baba yake marehemu Dkt.William Mgimwa.
Mkutano huo ulifanyika katika Kijiji cha Mseke na kuongeza kuwa, yeye ni Mhehe anayetokea katika familia ya marehemu Dkt. William Mgimwa, amezaliwa na kusomea Iringa lakini baadaye alibahatika kwenda masomoni nchini Uingereza na kupata shahada mbili za kitaaluma. 

“Mara ya mwisho kuitumia hati yangu ya kusafiria ilikuwa Desemba 2013 nilipokwenda Afrika Kusini kumuuguza marehemu baba yangu kabla mauti hayajamkuta. 

“CHADEMA hawana sera, katika shughuli zao za kisiasa kila siku wamekuwa wakipoteza muda mwingi kuzungumza habari binafsi za watu badala ya kujenga hoja za kuwasaidia Watanzania,” alisema. Alisema jimbo hilo limepiga hatua kubwa kimaendeleo lakini linachangamoto zake, hivyo akichaguliwa kuwa mbunge, kazi yake ya kwanza ni kumalizia utekelezaji wa Ilani ya CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015 na ahadi mbalimbali zilizoahidiwa na marehemu baba yake.

Bw.Mgimwa alisema kipaumbele chake cha kwanza ni elimu, pili kilimo, tatu miundombinu na mawasiliano ambapo hizo ni baadhi ya kazi ambazo atazifanya ili kuwaletea wananchi maendeleo. 
Katibu wa CCM Wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu, alisema katika kampeni hizo wakazi wa jimbo hilo wameshafanya maamuzi ya kuichagua CCM.

“Yapo mengi tumefanya kwa miaka mitatu iliyopita, tunatakiwa kupewa fursa ya kumalizia kazi tuliyoanza, mpeni kura zenu Bw.Godfrey Mgimwa amalizie ahadi za CCM,” alisema.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, alisema wanaoituhumu CHADEMA wakiihusisha na ubaguzi, hawakosei ndio maana kwa ubaguzi huo wamemkataa Mtanzania mwenzao na kudai si raia.
Alisema njia pekee ya kumaliza ubaguzi wa CHADEMA dhidi ya Watanzania wenzao ni kuwanyima kura katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Machi 16 mwaka huu na Uchaguzi Mkuu 2015.

Vyama vitatu vimesimamisha wagombea katika uchaguzi huo ambavyo ni CCM, CHADEMA kupitia mgombea wake Bi. Grace Tendega na Chausta ambacho kimemsimamisha Bw. Richard Minja.


No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...