WAZIRI WA TAMISEMI AKIFAFANUA JAMBO
SERIKALI kuu imefanya
maamuzi magumu yaliyoiachia halmashauri ya manispaa ya Iringa kilio chenye tiba
baada kuzuia mpango wake wa kujenga stendi mpya ya mabasi yaendayo mikoani
katika eneo linalolalamikiwa na wadau wa mazingira la Igumbilo, mjini Iringa.
Na wakati huo huo
imeipoza halmashauri hiyo kwa kuwaahidi kuchangia gharama mbalimbali
zitakazohitajika kufidia na kutathimini eneo mbadala watakalopata kwa ajili ya
ujenzi huo.
Zuio hilo lililokunja
sura za baadhi ya madiwani na watendaji wa manispaa hiyo “waliotaka kujua nani
atafidia gharama zao walizotumia katika mchakato mzima wa ujenzi wa stendi
hiyo” lilitolewa jana mjini Iringa kupitia matamko yaliyotolewa na mawaziri
watatu tofauti.
Waziri wa Maji,
Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Mazingira, Dk Binilith Mahenge na Waziri wa
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia kwa pamoja walitoa
ufafanuzi wa zuio hilo wakati wakizungumza na wanahabari ambao awali walizuiwa
kuingia kwenye kikao kilichokuwa kikipokea taarifa hiyo.
Mbali na mawaziri
hao, wajumbe wa baraza la madiwani la manispaa hiyo, sekretarieti ya mkoa wa
Iringa, wawakilishi wa vyama mbalimbali vya siasa, Baraza la Taifa la Usimamizi
wa Mazingira (NEMC) na wadau mbalimbali wa mazingira na maji walihudhuria kikao
hicho.
Akitoa taarifa ya
zuio hilo huku akishangaa kwanini wanahabari walizuiwa kuingia katika kikao
hicho, Waziri wa Tamisemi, Ghasia alisema tathimini ya pili ya athari ya
mazingira iliyofanywa na NEMC inahalalisha maamuzi hayo.
Alisema NEMC ilifanya
tathmini hiyo baada ya mdau namba moja wa eneo hilo linalopitiwa na mto Ruaha
Mdogo, Wizara ya Maji kupinga ujenzi wa stendi hiyo huku ikianisha sababu
mbalimbali.
Waziri Ghasia alisema
mto huo ndiyo chanzo pekee kinachohudumia jamii nzima ya wananchi wa manispaa
ya Iringa na hivyo kujenga stendi jirani yake kutaongza shughuli za kibinadamu
zinazoweza kuathiri mto huo na mazingira yake na hatimaye wanufaika wake.
Kwa kupitia mto huo
serikali kwa kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Iringa (IRUWASA) imewekeza
zaidi ya Sh Bilioni 70 ili kuwapatia wananchi maji safi na salama. Mradi huo
ulizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete Machi 22, 2012.
Ni katika mto huo
(mita kadhaa kutoka katika eneo linalopendekezwa kujengwa stendi) kuna mitambo
ya IRUWASA ya kupokea, kusafisha na kusambaza maji katika mji wa Iringa.
Alisema taarifa
iliyopo inaonesha kwamba ujenzi wa stendi hiyo utakwenda sambamba na ujenzi wa
huduma zingine zikiwemo gereji, hoteli na maduka hali inayoweza kuhatarisha
mazingira na usalama wa maji yam to huo.
“Kwahiyo tumewaeleza
rasmi ndugu zetu wa manispaa kwamba stendi hiyo haitajengwa katika eneo hilo
lakini kwakuwa wanayo mipango ya ujenzi huo utakaofadhiliwa na Benki ya Dunia,
watafute sehemu nyingine,” alisema.
Alisema serikali
inatambua gharama ambazo manispaa hiyo imeingia tangu ianze mchakato huo mwaka
2008 na ili kuponya machungu hayo itawajibika kutoa fedha zitakazohitajika kwa
ajili ya kuandaa eneo mbadala.
Naye Dk Mahenge
alisema; “sio jambo la ajabu kwa serikali kubadili maamuzi iliyoyafanya awali,
tumeamua hivyo baada ya kubaini kuwepo kwa baadhi ya mambo ambayo
hayakuzingatiwa wakati tathimini ya awali ikifanywa, mambo hayo ni pamoja na
athari za mabadiliko ya tabia nchi zinazoweza kutokea katika eneo hilo.”
Tathimini hiyo ya awali
ilifanywa na Mtaalamu Mshauri wa Mazingira aitwaye Arms on Environemnt Ltd ya
Dar es Salaam kwa gharama ya zaidi ya Sh Milioni 25 kama ilivyoelezwa katika
cha Kamati ya Fedha na Uongozi kilichofanyika Mei 2011.
Profesa Maghembe
alisema kumbukumbu zinaonesha kuwepo kwa mvutano wa ujenzi wa stendi hiyo tangu
mchakato wake uanzishwe mwaka 2008 kwahiyo kilichofanywa na serikali ni kwa
faida ya wananchi na Taifa kwa ujumla wake.
Dk Mahenge alisema
Oktoba mwaka jana na Februari 19 mwaka huu alipata malalamiko ya kimaandishi
kutoka kwa mdau namba moja wa maji ambaye ni Wizara ya Maji, akionesha hofu ya
wadau mbalimbali wa maji na mazingira endapo stendi hiyo itajengwa hapo.
Mbunge wa Jimbo la
Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema: “Suala hili sio la kisiasa hata
kidogo, ni suala la maendeleo ya watu, kwahiyo tuipongeze serikali kwa
kuzingatia ushauri uliotolewa na wataalamu wake, haya ndio maendeleo.
Mstahiki Meya wa
Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi alikataa kutoa mtazamo wake baada ya
kupokea uamuzi huo hata hivyo Waziri Ghasia aliingilia kati na kuitaka
halmashauri hiyo iendelee na mipango ya kujenga stendi kwa kutafuta eneo
lingine.
Kuzuiwa kwa ujenzi
huo, kulitabiriwa na wadau mbalimbali baada ya Februari mwaka huu, Dk Mahenge
kutembelea eneo hilo na kuiagiza NEMC kufanya upya tathimini hiyo huku
akiiagiza manispaa hiyo kusimamisha shughuli zote ilizokuwa imepanga kufanya
katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa
ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringabaada ya tathimini ya awali
kuonesha hakutakuwepo na athari za mazingira kama stendi hiyo itajengwa katika
eneo hilo, walipewa hati ya ujenzi Na.EC/E15/584 iliyotolewa Juni 15, 2012.
No comments:
Post a Comment