Thursday, August 29, 2013

MAKINDA APIGIWA DEBE KUGOMBEA URAISI 2015


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, asiyekuwa na wizara maalumu, Profesa Mark Mwandosya, amempigia debe Spika wa Bunge, Anne Makinda, akisema kuwa anafaa kuwa rais kutokana na sifa zake.

Profesa Mwandosya alimwaga sifa hizo bungeni jana, wakati akiunga mkono Azimio la Bunge la kumpongeza Makinda, kutokana na kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Chama cha Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CPA).


Profesa Mwandosya, ambaye miaka ya nyuma alijitosa katika kinyang’anyiro cha urais, alisema Spika Makinda ana sifa zaidi ya kumi ambazo zinamtosheleza kuwa rais na kwamba ni watu wachache wenye sifa kama hizo.

Akitaja sifa hizo, Profesa Mwandosya alisema Makinda ni mtu anayejiamini, mtenda haki, mchapakazi, mzoefu, msikivu, mbunifu, mwelewa, mvumilivu, mnyenyekevu na pia ni mtu mwenye msimamo.

Alisema kutokana na sifa hizo, Makinda anafaa kuwa kiongozi wa ngazi ya juu katika nchi, huku akimtazama kuwa ni mwanamke tishio katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

“Kwa namna ninavyomfahamu Spika Makinda ni tishio kwa uchaguzi wa rais mwaka 2015, kutokana na jinsi alivyokuwa na uwezo na mambo aliyowahi kulifanyia taifa hili.

“Kuchaguliwa kwake kuwa rais wa CPA ni hatua muhimu na nzuri kwa wanawake wengi kuongezeka katika Bunge la mwaka 2015 kwa kufikia asilimia 55, kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka,” alisema Profesa Mwandosya.

Profesa Mwandosya, ambaye amekuwa serikalini kwa muda mrefu, mwaka 2005 alikuwa miongoni mwa wanachama wa CCM waliojitokeza kuwania urais.Hata hivyo, kutokana na mchujo, Mwandosya alifanikiwa kuingia katika tatu bora. Wengine walikuwa ni Dk. Salim Ahmed Salim, Rais Jakaya Kikwete.

Naye Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah (CCM), alimwaga sifa kwa kiongozi huyo wa Bunge na kusema kuwa ni mwanamke shupavu atakayekuwa tishio katika uchaguzi mkuu ujao.

Akichangia mjadala huo wa kumpongeza Spika, Anna Abdallah, alisema Makinda ni mwanamke mwenye uwezo wa kuongoza nafasi yoyote ya juu, ikiwemo urais wa nchi.

Alisema kutokana na uzoefu wake katika uongozi hapa nchini, ameweza kuaminika hata nje ya nchi, jambo ambalo limemfanya kuchaguliwa kuwa Rais wa CPA.

“Kwa muda mrefu nchi yetu imekuwa ikihubiri juu ya mwanamke kupewa fursa na hasa kama ana uwezo, sasa wenzetu CPA wameweza kuliona hili wamemchagua,” alisema.

Mbunge huyo aliwataka wanawake kutojali maneno ya pembeni na sasa ni lazima jamii ikubali kumuamini mwanamke kwa kumpa nafasi ya juu ya uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Awali akisoma Azimio hilo la Bunge, Mwenyekiti wa CPA-Tanzania, Mussa Azzan Zungu, alisema Spika Makinda alishika wadhifa huo baada ya kufanyika kwa mkutano wa 44 wa chama hicho.

Zungu, ambaye ni Mbunge wa Ilala, alisema katika mkutano huo Bunge la Tanzania liliwakilishwa na wabunge wanane, akiwemo Spika Makinda na baadaye ulifanyika uchaguzi huo.

Chanzo:Mtanzania


No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...