Saturday, August 31, 2013

BAADHI YA MAONI YA CHADEMA KUHUSU KATIBA MPYA.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeeleza kuiunga mkono rasimu hiyo kwa asilimia 80 kulingana na maoni ya watu milioni 3.4 waliokusanya.Hata hivyo, CHADEMA imeainisha hoja 11 ambazo wananchi wamependekeza ziongezwe katika rasimu hiyo ya Katiba mpya.Akizungumza na waaandishi wa habari jana makao makuu ya chama hicho, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa alisema mrejesho huo umepatikana baada ya kuwazungukia wanachama wao na Watanzania wengine kwa wiki mbili.Dk. Slaa alisema maoni hayo yamekusanywa kupitia kanda 10 za chama hicho na Watanzania waishio nje ya nchi kwa njia ya kisayansi huku yakiwa na vithibitisho tofauti na vyama vingine vya kisiasa.Huku akieleza kuwa bado wanakusanya takwimu za Watanzania walioandika ambazo zinatoka mkoani, hadi jana walikuwa wamekusanya maoni kutoka katika mabaraza ya Katiba 117,274 yaliyoendeshwa na madiwani.Alisema kuwa waliendesha mabaraza ya wazi 3,200,889, ya ndani 130,004 na kukusanya maoni yaliyotumwa kwa njia ya barua pepe 612, ujumbe kwa njia ya simu za mikononi 12,345 na mitandao ya kijamii 1,681.Dk. Slaa alisema katika ziara hiyo, watanzania walisisitiza mambo 11 ambayo yapo katika rasimu hiyo na mapya kwa ajili ya kuongezwa kwa lengo la kuboresha rasimu hiyo kuwa ni pamoja serikali tatu yaani ya Jamhuri ya Muungano, Tanganyika na Zanzibar.Pili, ni kuitaja na kuiweka katika Katiba mpya mipaka ya Tanganyika na Zanzibar ili kudumisha amani ya nchi hizo na jirani zao.Kuhakikisha haki ya kila raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka 18 kupiga na kupigiwa kura katika uchaguzi wowote unaofanywa katika jamhuri.Hoja zingine ni swala la haki ya kupatiwa malipo ya uzeeni pamoja na msaada wa hifadhi ya jamii kwa gharama ya serikali wakati wa uzeeni, haki ya kupatiwa msaada wa matibabu, haki ya jamii kumiliki rasilimali za asili kama vile ardhi, madini, mafuta na gesi asilia, maji na misitu na wanyamapori vitumike kwa manufaa ya Watanzania.“Iwe marufuku kwa mamlaka ya serikali ya jamhuri za washirika wake kutwaa rasilimali asili kwa malengo ya kuzigawa kwa wawekezaji au kwa malengo yoyote bila ya kupata ridhaa huru na ufahamu wa wananchi wanaoishi kwenye eneo zinakopatikana rasilimali hizo,” alisema.Pia suala la uraia wa nchi mbili, mtu hatapoteza uraia wa Jamhuri ya Muungano kwa sababu tu ya kuwa na uraia wa nchi nyingine.Yapo pia masuala ya muungano yaani maadili na miiko ya uongozi na utumishi wa umma, haki za binadamu na wajibu wa raia, tume huru ya taifa ya uchaguzi na masuala yote yanayohusu uchaguzi.“Tume huru ya uchaguzi itatangaza matokeo ya uchaguzi wa Rais haraka iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kupita siku saba tangu tarehe ya uchaguzi huo.“Rais mteule atakabidhiwa madaraka ndani ya siku tisini baada ya kutangazwa kuwa ameshinda, wakati wote Rais akiwa madarakani na baada ya kuacha kushika madaraka hayo anaweza kushtakiwa kwa ajili ya kosa lolote la jinai chini ya sheria au chini ya mkataba wowote wa kimataifa ambao jamhuri ya muungano ni mwanachama,” alisema.Alitaja hoja ya kumi kuwa ni siku ya kupiga kura isiwe ni siku ya kuabudu ya imani ya dini yoyote ile, bali iwe siku ya kazi ambayo itapaswa kutangazwa kama siku ya mapumziko.Dk. Slaa alisema pamoja na ibara 68 za rasimu ambazo zimetolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, CHADEMA wakati inazunguka imekutana na mambo 11 hayo ambayo yalikuwa yakisisitizwa na wananchi.


No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...